
Cape Town
Cape Town (yaani “Mji wa rasi”, kwa Kiafrikaans: Kaapstad; kwa Kixhosa: iKapa) ni mji mkubwa wa tatu wa Afrika Kusini na mmoja kati ya miji mikuu mitatu ya nchi ikiwa ni makao ya Bunge. Pia ni mji mkuu wa jimbo la Rasi Magharibi (Western Cape / Wes-Kaap). Ni sehemu ya Jiji la Cape Town. Eneo lake ni km² 1,644 lenye wakazi 2,375,910 (mwaka 2005).


Jina la mji limetokana na Rasi ya Tumaini Jema iliyoko karibu na mji upande wa kusini.
. . . Cape Town . . .
Cape Town ni mji ambako bahari ya Hindi hukutana na Bahari ya Atlantiki. Uko kwenye latitudo ya 33.55° S (sawa na Sydney na Buenos Aires) na longitudo ya 18.25° E.
Ishara ya mji ni Mlima wa Meza unaotazama hori ya Cape Town ukitenganisha kitovu cha mji na makazi ya Cape Flats. Kitovu cha mji kiko kati ya mlima na bahari, sehemu yenye umbo kama la bakuli. Upande wa kusini iko rasi yenyewe, kama ulimi wa nchi wenye milimamilima kwa urefu wa kilomita 40.
Ng’ambo ya mlima kuna tambarare ya Cape Flats na hapo ni sehemu maskini zaidi za mji zenye wakazi wengi.
Cape Town ina uwanja wa ndege wa kimataifa mkubwa wa pili nchini. Ni mji wa Afrika Kusini unaotembelewa na watalii kushinda miji mingine yote. Wengi wanaona iko kati ya miji inayopendeza hasa kote duniani.
Kisiwa cha Robben Island kilikuwa mahali pa gereza alikofungwa Nelson Mandela; leo ni makumbusho yanayotembelewa na maelfu wa watalii kila mwaka.
Cape Town ni mji pekee Afrika ya Kusini wenye muingiliano mkubwa wa watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, hivyo kuufanya mji wenye mchanganyiko wa tamaduni nyingi kuliko yote Afrika Kusini.
Ukipita mitaa ya Wynberg utakutana na watu wengi wanaoongea lugha ya Kiswahili kutoka Tanzania, Kenya, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kiswahili ndiyo lugha kubwa ya kigeni ya Kiafrika inayozungumzwa sana Cape Town.
. . . Cape Town . . .