Abd el Kader

Abd el Kader (6 Septemba180826 Mei1883), (Kiarabu عبد القادر ابن محيي الدين ʿAbd al-Qādir ibn Muḥyiddīn; alijulikana pia kama Abdul Qadir, Emir Abdelkader au Abdelkader El Djezairi), alikuwa kiongozi wa kijeshi, wa kidini na wa kisiasa nchini Algeria.

Abd el Kader mnamo mwaka 1865

Alipigana dhidi ya uvamizi wa Ufaransa katika Algeria kuanzia mwaka 1830 hadi 1847. Baada ya kushindwa aliishi Dameski na hapo aliingilia katika ghasia ya mwaka 1860 alipookoa Wakristo wengi waliotishiwa na mauaji.

. . . Abd el Kader . . .

Abd el Kader alizaliwa mnamo 1807 au 1808[1] katika familia ya wataalamu wa Kiislamu walioamini walitoka katika ukoo wa mtumeMuhamad[2]

Tangu utotoni alianza masomo ya dini. Alipokuwa na miaka 14 alifikia hadhi ya hafizi (mwenye kukariri kurani yote) na mwaka 1825 aliondoka kuelekea Makka kwenye safari ya hajj. Safarini aliongeza elimu yake akavutiwa na matengenezo ya Muhammad Ali Pasha aliyoyaona wakati alipopitia Misri. Alirudi Algeria miezi michache kabla ya uvamizi wa Kifaransa.

Eneo la dola la Abd el Kader mnamo 1838

Mwaka 1830 Algeria ilivamiwa na Ufaransa na utawala wao ulichukua nafasi iliyowahi kuwa mikononi mwa Waosmani kwa miaka 300. Wakati wa jeshi la Ufaransa kufika Oran katika Januari 1831, baba yake Abd el-Kader aliongoza majaribio ya upinzani chini ya bendera ya jihadi.

Baada ya Wafaransa kutwaa miji mikubwa wapinzani walikutana mlimani na hapo Abd el-Kader alichaguliwa kuwa kiongozi kwa cheo cha “amir”. Katika muda mfupi alifaulu kuunganisha makabila ya Algeria ya magharibi chini ya uongozi wake.

Mwaka uliofuata (1834) jenerali Mfaransa Desmichels alipaswa kumtambua kama mkuu wa eneo la Oran. Patano hili liliongeza heshima yake kati ya makabila ambayo hadi hapo yalikataa kuchukua msimamo.

Hadi mwaka 1839 kulikuwa na kipindi cha amani ambapo Abd el-Kader alipanua himaya yake katika milima ya Atlas na ng’ambo hadi vyanzo vya jangwa kubwa la Sahara. Aliweka misingi ya dola lenye jeshi la kudumu na pesa yake. Mwenyewe aliishi maisha ya kawaida akikaa katika hema. Alikataa kutumia cheo cha sultani akikazia hadhi yake ya kitaalamu.

Abd el Kader alisalimu amri (mchoro wa Kifaransa)

Kipindi cha amani kilikwisha wakati gavana mpya wa Kifaransa aliamua kupeleka walowezi katika eneo la Abd el Kader aliyewashambulia tarehe 15 Oktoba1839. Kipindi cha vita kilifuata ambapo Wafaransa waliongeza idadi ya wanajeshi wao na kutumia mbinu kali dhidi ya makababila yaliyomsaidia Abd el Kader. Wafaransa walichoma nyumba na mazao yote wakafaulu kuvunja upinzani kwa silaha ya njaa.

Abd el Kader alivuka mpaka wa Moroko lakini Wafaransa walivamia upande ule pia. Hatimaye alilazimishwa kusalimu amri tarehe 21 Desemba1847. Alikubali kukamatwa na na Wafaransa kwa ahadi ya kwamba watampeleka Misri. Lakini alipelekwa Ufaransa na kushikwa huko pamoja na familia yake.

Baada ya miaka 5 rais mpya wa Ufaransa Louis Napoleon Bonaparte alimweka huru, akampatia pensheni na kumruhusu kuhamia Milki ya Osmani.

. . . Abd el Kader . . .

This article is issued from web site Wikipedia. The original article may be a bit shortened or modified. Some links may have been modified. The text is licensed under “Creative Commons – Attribution – Sharealike” [1] and some of the text can also be licensed under the terms of the “GNU Free Documentation License” [2]. Additional terms may apply for the media files. By using this site, you agree to our Legal pages . Web links: [1] [2]

. . . Abd el Kader . . .

Previous post Nimefulia
Next post Siti Binti Saad