Nehemia

Nehemia (kwa Kiebraniaנְחֶמְיָה yaani: “Faraja ya Mungu” au: “Aliyefarijiwa na Mungu”), ni mtu wa Biblia, mhusika mkuu wa kitabu chenye jina lake.

Picha takatifu ya Nehemia.

Aliishi katika karne ya 5 KK.

. . . Nehemia . . .

Alikuwa mwana wa Hachaliah (Nehemia 1:1), na familia yake ilikuwa inaishi Yerusalemu (Nehemia 2:3) wakati ambapo mji huo ulikuwa chini ya dola la Waajemi.

Nehemia, kisha kuwa afisa wa Kiyahudi katika nyumba ya mfalme, alipandishwa cheo kuwa mnyweshaji mkuu wa mfalmeArtashasta I katika ikulu la Shushan akafunga urafiki naye (Neh 1:11).

Wayahudi waliposikia kwamba mmojawao anaweza kusema na mfalme, walifika Uajemi ili wamwone. Nehemia aliposikia kwa ndugu yake Hanani na wengineo juu ya hali duni ya mji mkuu wa Yudea alisikitika sana, akafunga na kusali. Alijua kwamba matatizo ambayo yeye na watu wake waliyapata yalikuwa matokeo ya dhambi zao, na kwa moyo wa unyenyekevu na kukiri dhambi, aliweka mambo yote mbele ya Mungu na kuomba msaada wake (4-11).

Kwa muda wa miezi minne Nehemia aliomba kuhusu mambo hayo. Kwa hiyo alikuwa tayari kumweleza mfalme shida zake, nafasi ilipotokea ghafla.

Matokeo yake ni kwamba, mfalme aliona huzuni yake akamuuliza imetokana na nini. Nehemia akajieleza akaruhusiwa kwenda Yerusalemu kama tirshatha, yaani liwali, na kushughulikia ujenzi wa ngome wa mji na ustawi wa Wayahudi wote wa eneo hilo. Pia alipewa vifaa vilivyohitajika (2:1-8).

Nehemia alipokwenda Yerusalemu, hali na mazingira yalikuwa tofauti na wakati wa safari ya Ezra, naye aliona vizuri kupokea msaada wa mfalme, yaani kusindikizwa na kundi la askari (9; taz. Ezra 8:21-23). Maafisa wengine waliokuwa wametawala eneo la Yerusalemu hapo awali, walikasirika na kugeuka kuwa maadui wakali walipogundua kwamba eneo hilo liliwekwa chini ya liwali Nehemia. Licha ya kuwa Myahudi, alikuwa na mamlaka kutoka kwa mfalme wa Uajemi, na hivyo hawakuweza kumwingilia tena (10).

Kujenga upya kuta kubwa zilizobomolewa ilikuwa kazi ngumu sana, tena kubwa mno, hata wengine walisema haiwezekani. Kwa hiyo, kabla ya kutangaza madhumuni yake, Nehemia alichunguza mambo yote kwa siri, ili ajue vizuri kazi iliyotakiwa na vifaa vilivyohitajika (11-16). Ujuzi huo ambao Nehemia alijipatia, pamoja na maelezo yake ya jinsi Mungu alivyoongoza mambo yote mpaka alipotumwa Yerusalemu, yaliwaaminisha watu kwamba wakati umewadia wa kuanza kujenga ngome, wasiogope upinzani ambao utaendelea kuwepo (17-20).

Kazi ilipangwa vizuri. Vikundi mbalimbali vya watu vilipangwa kila mahali bega kwa bega kuzunguka mji wote, hata kuta zote ziiweza kujengwa wakati mmoja. Orodha ya wafanyakazi inaonyesha kwamba Wayahudi kutoka mbali na karibu walikuja kusaidia. Si waashi tu, bali pia makuhani, mafundi wa dhahabu, mafundi wa manukato, maafisa wa serikali, wafanya biashara na hata wanawake walisaidia kazi hiyo (3:1-16). Walawi walijenga karibu na nyumba ya kuhani mkuu (17-21). Makuhani na watu wengine walioishi Yerusalemu, kwa kawaida walipangiwa sehemu za karibu na nyumba zao, na watu waliotoka mbali walijenga sehemu zilizobaki (22-32).

Wayahudi walikuwa na kibali cha mfalme wa Uajemi kwa mradi wa kujenga kuta, kwa hiyo wapinzani wao ambao pia walikuwa chini ya mfalme huyo, waliogopa kuwashambulia hadharani. Hata hivyo waliwadhihaki na kufanya mzaha juu ya kazi yao, wakitumaini kwamba wataweza kuwachosha na kuwaachisha kazi ya ujenzi (4:1-5).

Lakini Wayahudi hawakukatishwa tamaa haraka wakaendelea na kazi yao (6). Kwa hiyo maadui walikusudia kuleta machafuko na kuvuruga akili za Wayahudi kwa kuleta mashambulio ya siri sehemu mbalimbali mjini. Wayahudi waliposikia makusudi hayo walizidisha maombi na kuongeza ulinzi wao (7-9). Wale walioishi vijijini walimletea Nehemia habari kuhusu shughuli za maadui (10-12), lakini Nehemia hakuogopa hatari. Aliwapa wafanyakazi silaha na kuwagawa katika makundi mawili. Wengine walipofanya kazi wenzao walilinda. Maarifa ya kivita yalifikiriwa ili kujihami kama maadui watashambulia ghafla (13-21). Watu wa nchini waliofanya kazi Yerusalemu waliombwa kulala mjini bila ya kurudi nyumbani, kwa kusudi la kuongeza ulinzi wa usiku (22-23).

Tatizo lingine lililomkabili Nehemia lilikuwa hali ya manung’uniko yaliyoongezeka polepole na kwa muda mrefu baina ya matajiri na maskini. Watu waliokuwa na shida ya fedha walikopa kwa matajiri ili waweze kununua chakula na kulipa kodi zao kwa serikali ya Uajemi. Matajiri wakaona hali hiyo kuwa ni nafasi ya kupata faida kwa kuwadai watu riba kubwa. Kisha maskini waliposhindwa kulipa, matajiri walichukua mashamba yao kuwa malipo ya deni, au wakachukua hata watoto wao na kuwafanya watumwa. Shida hiyo ilizidi katika mwaka wa njaa na wakati wa kazi ya kujenga kuta, kwa sababu wafanyakazi hawakuweza kujipatia mishahara ya kawaida. Maskini hawakuona njia yoyote ya kuondokana na hali hiyo, wakamsihi Nehemia awasaidie (5:1-5).

Nehemia alijua uchoyo na hila za matajiri, kwa sababu siku moja aliwaona wakiuza Wayahudi wawe watumwa wa wageni, nao walijua kwamba ilikuwa siasa ya Nehemia kuwanunua watumwa wale tena na kuwapa uhuru (6-8). Kwa hiyo aliamuru kwamba vitu au watu waliochukuliwa kuwa malipo ya madeni warudishwe na kupewa uhuru, na riba juu ya mikopo iondolewe kabisa (9-13).

Muda wote wa miaka 12 ya uliwali wake, Nehemia aliwapa watu kielelezo kizuri ili wakifuate. Yeye hakudai kitu chochote alichostahili kufuatana na cheo chake, asije akawatwisha watu mzigo zaidi. Aliwalisha wageni na wafanyakazi wake hata kutoka mfukoni mwake mwenyewe (14-19).

Maadui walipoona kuta zikikaribia kumalizika, waliona njia ya pekee ya kuzuia kazi hiyo ni kumwondoa Nehemia mwenyewe. Walijaribu kumwita katika vijiji vya mbali ili wakamwue huko, lakini Nehemia alitambua hila yao (6:1-4). Kisha wakaeneza fununu kwa njia ya barua wazi iliyosema kwamba Nehemia alipanga maasi dhidi ya Uajemi, lakini kazi yao ikawa bure (5-9).

Maadui wakafikiri maarifa mengine tena. Walijaribu kumsababisha Nehemia afanye mambo ambayo yataharibu sifa yake ya kuwa mtu asiyeogopa wapinzani naye avunje heshima ya hekalu. Mara nyingine tena wakashindwa (10-14). Hata wapelelezi na wasaliti ambao maadui walikuwa wamewaweka mjini Yerusalemu hawakuweza kumzuia Nehemia kumaliza kazi yake ya kujenga ukuta (15-19).

Wakati huo Yerusalemu ulizungukwa na kuta imara ulioweza kulinda mji. Hata hivyo, Nehemia alitaka kuongeza usalama. Mji ulikuwa haujapata wenyeji wengi, kwa hiyo tahadhari ilitakiwa. Ili kuzuia mashambulio ya ghafla ya alfajiri, Nehemia aliagiza milango ya mji isifunguliwe mpaka watu wote wawe macho na katika shughuli zao za kawaida za mchana. Pia aliweka ulinzi wa ngome yote uliopangwa kwa maarifa, ili watu wa kila nyumba walinde karibu na eneo lao (7:1-4).

Kisha Nehemia akaandika orodha kubwa ya watu wote walioishi Yerusalemu. Orodha hiyo ililinganishwa na ile ya kundi la kwanza la watu waliorudi kutoka uhamishoni pamoja na Zerubabeli karibu miaka 100 iliyopita (5-73; taz. Ezra 2:1-70, ambapo orodha hiyo imeandikwa).

. . . Nehemia . . .

This article is issued from web site Wikipedia. The original article may be a bit shortened or modified. Some links may have been modified. The text is licensed under “Creative Commons – Attribution – Sharealike” [1] and some of the text can also be licensed under the terms of the “GNU Free Documentation License” [2]. Additional terms may apply for the media files. By using this site, you agree to our Legal pages . Web links: [1] [2]

. . . Nehemia . . .

Previous post Alberto Mkuu
Next post Usultani wa Zanzibar