
Barabara ya hariri
Barabara ya hariri (kwa Kiingereza: “Silk road”) ilikuwa njia muhimu ya biashara kati ya China kwa upande mmoja na Afrika Mashariki, Mashariki ya Kati halafu Ulaya kwa upande mwingine. Biashara hiyo iliendelea tangu karne za kabla ya Kristo.

Jina la “barabara ya hariri” limetokana na hariri ambayo kwa muda mrefu ilitengenezwa katika China pekee ikawa kati ya bidhaa zilizotafutwa sana duniani kwa bei ya juu.
Mnamo Juni2014, UNESCO imetangaza sehemu Chang’an-Tianshan ya barabara hiyo kuwa mahali pa Urithi wa Dunia.
. . . Barabara ya hariri . . .
Barabara ya hariri haikuwa njia moja tu bali jumla ya njia za misafara kati ya China na nchi za Magharibi zilizopita katika Asia ya Kati.
Kulikuwa na njia za kando, hasa baharini, kati ya China na Uhindi halafu kutoka Uhindi hadi Irak au Misri. Njia za bahari zilikuwa muhimu hasa kama njia ya nchi kavu ilikatika wakati wa vita au ukosefu wa usalama. Kuna vipindi vichache ambako eneo lote la barabara ya hariri lilikuwa na usalama, hasa wakati wa utawala wa Wamongolia. Vinginevyo safari zilikuwa za hatari zikachukua muda mrefu. Bidhaa zilipita mikononi mwa wanafanyabiashara mbalimbali zikaongezewa bei njiani.
Si bidhaa tu ndizo zilizosafiri kwenye barabara ya hariri. Wasafiri, sanaa, mawazo, mafundisho, dini na magonjwa walipita pia kwa njia hiyo.
Teknolojia kama za kutengenezwa kwa karatasi au kuchapishwa kwa vitabu zilipita njia hiyo kutoka China hadi Asia ya Magharibi na kutoka huko hadi Ulaya.
Uenezaji wa Ubuddha kwenda Mongolia na China katika karne ya 1BK, wa Ukristo kufika China katika karne ya 3 na wa Uislamu kuelekea mashariki katika karne ya 8 ulifuata barabara hii.
Magonjwa yalipita njia hiyohiyo. Kwa mfano tauni ilianza katika miaka ya 1330 katika China kwenye jimbo la Yunnan. Ugonjwa huu unategemea viroboto kama kituo cha virusi vyake. Farasi za jeshi la Mongolia na biashara ya ngozi ilipeleka viroboto wale hadi Bahari Nyeusi. Mwaka1348 wafanyabiashara Waitalia kutoka Bahari Nyeusi waliingiza ugonjwa Ulaya yenyewe ulikoua robo ya wakazi wote.
. . . Barabara ya hariri . . .