Hassan bin Omari

Hassan bin Omari (au Makunganya[1]; alifariki 26 Novemba1895) alikuwa MyaoMwislamu wa Makanjila, aliyeishi mlimani, na aliyefanya biashara ya pembe za ndovu na ya watumwa, na pia kushambulia misafara iliyopita katika eneo lake la Mavuji, karibu na Kilwa Kivinje. Baada ya kupigana na Wajerumani alikamatwa, na mwishowe alinyongwa na Wajerumani, pamoja na wenzake.

Hassan bin Omari (aka Makunganya), kulia, Omari Muenda, katikati na Jumbe, kushoto

. . . Hassan bin Omari . . .

Kufahamu asili yake ni kuelewa sababu za uasi wake dhidi ya Wajerumani wa Afrika Mashariki wakati huu, pamoja na wengine dhidi ya Waingereza katika bara la Afrika. Hatuna maandiko mengi zaidi ya kihistoria ya wakati huu ila yale ya wazungu waliotawala nchi. Asili ya Hassan bin Omari katika watu wa kabila ya Makanjila Yao[2] ambao, kufikia karne ya 19, walikuwa wasimamizi wa njia kuu ya misafara ya biashara kutoka nchi za Nyasa na majirani ya mto wa Zambezi, mpaka pwani ya kusini ya Tanzania ya leo, hasa mji wa Kilwa Kivinje, kilomita 25 kaskazini mwa Kilwa Kisiwani, ambapo watu wengi Wayao walikuwa wamekwisha kuanza kuishi. Kilwa Kivinje ilikuwa bandari kuu ya usafirishaji wa watumwa na wa bidhaa mbali mbali katika eneo la Kilwa wakati wa utawala wa Omani na Ujerumani.

Deutsch Ostafrika

Hassan bin Omari alishirikiana na watu Wayao wengine katika mapigano ya 1888. Pia, idadi kubwa ya Wayao katika karne hiyo tayari walifuata dini ya Uislamu. Biashara enyewe baina ya Uyao na Kilwa, pamoja na baina ya nchi za kusini mbele ya kisiwa cha Msumbiji, ilianza kabla karne ya 17. Misafara ya biashara hii ilifika Kilwa kila mwaka kuleta pembe za ndovu, watumwa na bidhaa zingine.[3]

“Historia ya Kilwa Kivinje” tunaambia kwamba Wayao walikuwa watu wa bara wa kwanza kukaa katika Kilwa Kivinje[4].

Makanjila III, mfalme wa Mangochi Nyasa mnamo 1870, alikaribisha Uislamu kuwa dini yake binafsi, na ya baraza yake. Pamoja na viongozi wengine Wayao, walihusika sana kukamata watu wa makabila majirani na kuwatia utumwani. James Frederic Elton mnamo Septemba, 1877 alisimulia kwamba Makanjila ni “… chifu mkuu wa biashara ya watumwa katika pwani ya mashariki ya Nyasa”. Aliendelea kusema, aliona “nchi iliyolimwa vizuri … na nyumba zilizojengwa kwa uangalifu sana… Mkuu mwenyewe anaye veranda na ‘baraza’ ya ukubwa kupita nyumba nyingi za Zanzibar”.[5] Pia, Makanjila alionyesha heshima ya Sultani wa Zanzibar, kama aliyemwambia Johnson mnamo 1890, “Wazungu wangekuja kutwaa nchi ya Sultani wa Zanzibar, mimi, Makanjira, nitamwokoa!”[6]

Lakini, katika karne ya 19, vikosi vya Ujerumani na Uingereza vilipigana na wenyeji wengi kwa sababu ya kuondoa biashara hii ya utumwa mpaka mwisho, biashara ambaye ilikuwa ya faida kubwa kwa watu kama Wayao. Wakati ule ule wa kutua Wajerumani kwa pwani ya Afrika Mashariki mnamo 1888 kutweka bendera zao, na manowari za Ujerumani na zingine za Ulaya zilizolinda miji ya pwani, Wayao waliteswa na kampuni na vikosi vya Uingereza dhidi eneo lao katika mkoa wa Nyasa. Harry Johnston, pamoja na kikosi chake cha wanajeshi wa Sikhi na wa Zanzibar, kwa maneno yake akajulisha kwamba “ongezeko kubwa la nguvu nilizonazo ziliniwezesha, katika msimu wa vuli wa 1893, kutekeleza ushindi kabisa wa Makanjira. Tulimfukuza kwanza kutoka pwani ya magharibi ya ziwa…na kisha kumshambulia katika nchi yake na kuteka kila moja ya miji yake kwa mfululizo”.[7]

Tunaweza kutambua pia kwamba Makanjila, wakati huu, alikuwa Mwenchande Salimu ambaye, baada ya kushindwa mikononi mwa Johnston, alikimbilia “Mwembe kwa rafiki yake Che Mataka, mwenzake; baadaye alijiunga na Che Makunganya mrimani(ambapo alikaa) hadi mnamo 1914 aliporudi.”[8] Angalifika pwani mnamo 1894 au 1895, angekuwa pamoja na Makunganya, yaani Hassan bin Omari, wakati huo.

. . . Hassan bin Omari . . .

This article is issued from web site Wikipedia. The original article may be a bit shortened or modified. Some links may have been modified. The text is licensed under “Creative Commons – Attribution – Sharealike” [1] and some of the text can also be licensed under the terms of the “GNU Free Documentation License” [2]. Additional terms may apply for the media files. By using this site, you agree to our Legal pages . Web links: [1] [2]

. . . Hassan bin Omari . . .

Previous post Edith Masai
Next post Milipuko ya Mabomu – Mbagala